Friday, 23 October 2015
Monday, 19 October 2015
UCHAMBUZI WA MASHAIRI YA MALENGA WAPYA (BY MWL VITUS M. JOHNSON)
UHAKIKI WA MASHAIRI YA MALENGA WAPYA
\MWANDISHI:
TAASISI YA KISWAHILI, ZANZIBARWACHAPISHAJI: OXFORD UNIVERSITY PRESS
MWAKA: 2001
JINA LA KITABU
Jina la kitabu linasadifu yaliyomo katika kitabu. Kwa upande wa maudhui mambo yanayoelezwa mengi yanaigusa jamii ya sasa. Masuala ya maadili, siasa, uchumi, ukombozi wa kiutamaduni changamoto na suluhisho ya matatizo yanayoikumba jamii yanaendana na wakati wa sasa. Hivyo upya wa malenga wapya ni kweli. Kifani pia Malenga wapya wameweka muundo na mtindo wa kisasa.
Malenga wapya ni kitabu
kichaozungumzia masuala mbalimbali ya kijami kama vile ukombozi wa mwanamke,
umuhimu wa kilimo, umhumimu wa kuondoa matatizo katika jamii, ukombozi wa
mwanamke, umuhimu wa kilimo na kadhalika.
MAUDHUI
A : DHAMIRA
1)
Suala la
uongozi bora na uwajibikaji
Suala la uongozi limejadiliwa katika
pande zote mbili za uongozi mzuri na uongozi mbaya. Waandishi wameonesha yote
haya wakiwa na lengo la kuikomboa jamii. Wamesisitiza kuhusu uongozi bora mfano
katika shairi la “Payuka” anawaasa viongozi kuwa watekelezaji wa yale
wanayoyaahidi na sio kuwa wapayukaji tu. Mfano ubeti wa pili anasema
“Kupayuka kwenu huko,
Mbona
tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.”
Pia katika shairi la “Puuzo”
anawakanya viongozi wasiowajibika kutekeleza majukumu yao na kuacha uzembe.
Anawaasa kujituma na kufanya kazi kwa bidii kwani ni wajibu wao. Anasema katika
ubeti wa kwanza
“Ofisini ukifika, wajitia pirika,
Haja unayoitaka mwenyewe tahangaika,
Wajifanya
hawajali.”
2)
Ukombozi
wa kiuchumi
Mwandishi anaona kuwa ili jamii
ikomboke kiuchumi yapo mambo ya msingi kutekelezwa. Miongoni mwa mambo hayo ni
kufanya kazi kwa bidii na kuacha uvivu. Mfano katika shairi la “Charuka”
tunaambiwa kuwa,
“Charuka baba haraka, na mfano
kuonyesha,
Charuka upate vuka, mikondo hii maisha, Charukeni
kina kaka, na dada nawaamsha,
Basi tena kulegea, charuka chacha rukaka.”
Pia anakazia suala la kilimo kama
ndio msingi wa kujikomboa kichumi katika shairi la “Adui” na katika
shairi la “Mkulima”anaonesha umuhimu wa kumthamini mkulima na kilimo.
Vikiwa kama vigezo vya maendeleo nchini mwetu. Mfano katika shairi la “Adui”
anasema;
“Tulime jama tulime,
tushinde adui njaa,
Hapa kwetu ituhame, kwingine kutokomea,
Wala sisi tusikome, chakula kujilimi
Tutie
jembe mpini, tuteremke shambani”.
Pia katika shairi la “Tuyazingatie
haya” mwandishi anataja mambo ambayo anaamini kuwa yakizingatiwa yataweka
uchumi kuwa imara kama vile, kuchapa kazi, kukomesha ubaguzi kutopora mali za
serkali, kushirikiana, kukosoana na kuepuka tamaa. Mfano ubeti wa pili anasema;
“Uchumi kuufufua, si hotuba refu
sana,
Moja litalosaidia, ni kwa kuhamasishana,
Jengine lafuatia, sote kushirikiana,
Tuyazingatie
haya, wala tusirudi nyuma.”
3)
Ukombozi
wa mwanamke
Mwandishi kwa kutambua nafasi muhimu
ya mwanamke katika jamii, hakusita kuikumbusha jamii juu ya kuwaheshimu,
kuwathamini, kuwapa uhuru na kupinga tamaduni zote zinazomkandamiza mwanamke.
Anaamini kuwa kumkandamiza mwanamke ni kuikandamiza jamii. Anayazungumzia haya
katika shairi la “Kifungo”, “Hina inapapatuka”, “Raha”. Mfano katika
shairi la “kifungo” ubeti wa saba anasema;
“Kwa kuwa mwanamke, ndani
mnanifutia,
Lazima nje nitoke, kupata ninayotaka,
Nimechoshwa na upweke ,
sitaki kudhalilishika,
Kifungo kimenichosha, minyororo nafungua.”
Pia katika shairi la “Hina
inapapatuka” anawahamasisha wanawake kukazana na kushikilia vipaumbele vya
maendeleo, anasema:
Nasaha ninatamka, mabibi
nawaambia,
Uzi mulioshika, msije kuwaachia,
Ogopeni kina kaka, yenu nkutowavunjia,
Unyonge
inaondoa, hina inapapatuka”.
4)
Suala
maadili mema na maonyo
- Umuhimu Wa kuwa na kauli nzuri
Mwandishi katika shairi la “Ulimi”
anawaasa watu kuwa ulimi mzuri kwa maana ya kuongea vizuri na watu kwa adabu,
na heshima. Anaona kuwa ulimi ni kiungo kidogo lakini kinaweza kusababisha
matatizo au mambo mazuri. Anauasa ulimi akisema;
“Usiropokeropoke, kwa wenzio kwanza
sema,
Usipachikepachike, maneno yasiyo mema,
Useme wanufaike kwa kauli yako njema,
Ewe
ulimi sikia!
- Umuhimu wa kutenda wema kwa binadamu wenzetu
Mwandishi anaona kuwa wanajamii
wanapaswa kutenda wema kwa wanajamii wenzao kwani matokeo ya wema ni mafanikio
na shukrani. Anasema katika shairi la “Hisani hulipwa”
“Akuulizae, uwapo na shida,
Akuteteae ukishambuliwa, Akumurikae,
uwapo na giza,
Hisani
hulipwa
- Umuhimu wa kuwa na subira katika maisha
Mwandishi anawaasa wanajamii
kutokurupukia maisha hasa vijana. Katika shairi la “Siharakie maisha”
Anaona upo umuhimu wa kufanya mambo kwa wakati na kuacha tamaa kwani kila jambo
na wakati wake. Anawaasa wanafunzi kushikilia masomo na kutolimbukia mambo
ambayo si wakati wake. Anasema; “Punguza
haraka zako,
Badilisha
mwendo wako,
Subira ni chombo chako,
Takutwisha
kwenye fuko,
Usisahau
usemi, subira yavuta heri.”
- Umuhimu wa kuishi vyema duniani
Katika shairi la “Ulimwengu”
na “Maisha ni kama njia” mwandishi anaiambia jamii kuishi vizuri katika
dunia kwani dunia ni mapito tu. Mfano katika shairi la “Maisha ni kama njia”
anasema:
“Iweze yako suduri, binadamu
zingatia,
Kaa
kutafakari, utende yalo sawia,
Ubabe au kiburi, havitokusaidia, Maisha
ni kama njia, tukumbuke akhiria”.
Pia katika shairi la “Ulimwengu”
mwandishi anawaambia wanajamii kuwa katika dunia kuna mambo mengi mabaya na
mazuri hivyo ni budi kuyavumilia na kuendanana nayo vizuri. Anasema ubeti wa
nne;
“Umbile vile lilivyo, ni umbo la
mitihani,
Usilendeshe visivyo, litakupa hamkani,
Ambaa hebu rudivyo, ulimwengu ni shetani,
Ulimwengu!
- Uaminifu katika ndoa
Suala la ndoa kwa jinsi anavyosema
mwandishi uaminifu ndio jambo la msingi kwani huleta upendo na amani kwa
familia. Anawashauri wanaume kujali familia zao na kuwa na mahusiano mengine
nje ya ndoa. Katika shairi la “Kwanini” anasema;
“Mke wake, atamwacha, singizini,
Atoroke, parakacha, migombani, Kumbe
kake, anakocha, mwa jirani,
Kwanini?”
Mume
pesa, apeleke, chumbageni,
Azitesa, toto zake, firauni,
Apepesa,
mwendo wake, ulevini,
Kwanini”.
- Matumizi mazuri ya pesa
Mwandishi anaona upo umuhimu wa
kutofuja pesa. Anashauri watu kuwa na utamaduni wa kuweka akiba. Anaona kuwa
ufujaji pesa ni dhambi na si haki. Katika shairi la “Israfu”
“Mali ulojichumia,
Ni yako nakubalia,
Lakini kiangalia,
Vipi
unaitumia,
Mwenzangu nakuusia, israfu haifai.”
- Kuzingatia dini na kumuabudu Mungu
Mwandishi anawaasa wanadamu kutii
maadili ya dini zao. Kwani misingi ya dini huelekeza watu katika mema. Anasema
haya katika shairi la “Maisha ni kama njia”. Ubeti wa tano anasema;
“Tamati nawashauri, tumuabudu
jalia
Ibada na tukithiri, na kutenda yenye njia,
Twenda
kila mahali shubiri, hukumu yatung
Maisha ni kama njia, tukumbuke akhiria”
5)
Suala la
Mapenzi
Katika shairi la “Ua” na
katika shairi la “Nipate wapi mwingine” waandishi wanaona kuwa mapenzi
ya dhati na ya kweli ni jambo jema. Anawataka watu kuthamini na kuwaheshimu
wapenzi wao na binadamu wengine. Mfano katika shairi la “Ua” anasema;
“Ua limejituliza, mtini laning’inia,
Mwenyewe laniliwaza, furahani laniti
Ua
sasa limepea, macho walikodolea.”
Pia katika shairi la “Nipate wapi
mwingine” mwandishi anazungumzia jinsi ilivyo kazi kupata mpenzi wa kweli.
Dunia sasa imebadilika watu hupenda vitu vingine badala ya kuwa na mapenzi ya
kweli yanayojali utu wa mtu. Mwandishi anayaita kuwa hayo ni mapenzi ya
ulaghai. Mashairi ya “Utanikumbuka” linaasa juu ya usaliti katika
mapenzi kuwa haufai. Shairi la “Kuunge” na “kitendawili”
yanakazia zaidi juu ya kuwa na msimamo katika mapenzi. Anafananisha watu wasio
na mapenzi ya kweli na Njiwa anayerukaruka asiyetulia. Mwandishi anasema;
“Wapo wafugaji tele, madebe
wamepachika,
Na
njiwa wapo milele, watu hawendi kutaka,
Kutwa waweka kelele, wapanda mara kushuka, Njiwa
ameshanitoka, nipate wapi mwingine”.
Mwandishi anayaita kuwa hayo
ni mapenzi ya ulaghai
6)
Umuhimu wa
wosia
Suala la kutoa wosia kwa mwanadamu
ni jambo la muhimu sana pindi anapokufa. Suala hili huepusha migogoro na
malumbano kwa wanafamilia wanaobaki. Katika shairi la “Nini wanangu”
anasema:
“Shikamaneni wanangu, siku yangu
ikifika.
Mutamakani
kichungu, musije kutawanyika,
Kiondoeni kizungu, mshike mliposhika, Sizidi
nasaha zangu!”.
7)
Suala la
ukombozi wa kifikra
Mwandishi anaitaka jamii kukomboka
kifikra. Mambo haya anayazungumzia katika shairi la “Usiwe bendera”.
Suala la kuwa na msimamo binafsi na thabiti katika maamuzi ya mambo ni jambo la
msingi katika maisha ya kila siku. Anaona kuna athari ya kuendeshwa au
kuamuliwa mambo kama bendera inavofuata upepo. Mfano;
“Tumia zako fikrazo, pima yanofaa, Tazama
kikwazo, wapi chatokea,
Pima na uwezo,
wakukifanyia,
Usiwe bendera, kufata upepo”.
8)
Utetezi wa
haki
Mashairi ya “Mpaka lini”, “Samaki
mtungoni” “Sokomoko” yanazungumzia juu ya ukosefu wa haki. Mahali popote
hapawezi kuwa na amani bila kuwepo haki. Hivyo mwandishi anaeleza:
“Msema kweli, kwenu ninyi ni
chagizo,
Mtaka
hali, havuki mbele ya vikwazo,
Mwongo sana, kwenu ninyi ni kigezo, Mpaka
lini mtatuchezea?”
Katika shairi la “Samaki
mtungoni” mwandishi anaona kuwa kwa sababu ya ukosefu wa haki watu
hudhulumiwa na kuteswa anafananisha wadhulumu haki na wavuvi anasema:
“Haki yao mepotea, na heshima
kuondoka,
Mebaki waning’inia, mtungoni mepangika, Bwana amechachamaa,nyumbani kwenda kupika,
Leo wako mtungoni, huzuni imewakumba.
9)
Utabaka na
unyonyaji na unyanyaswaji
Mambo ya matabaka ndiyo
yanayochangia kunyanyaswa, kunyonywa na kukandamizwa. Matabaka ambayo waandishi
wanayazungumiza ni matabaka ya kiuchumi, kijamii na kisisasa. Katika shairi la “Samaki
mtungoni” samaki anachorwa kama mtu mnyonge na mvuvi akiwa ni mwenye
mabavu. Anaonesha jinsi watu wasivokuwa na uhuru bali kukandamizwa na kuteswa.
Hili limewekwa wazi ili kupiga vita mambo hayo katika jami. Anasema:
“Huzuni imewakumba, raha zao kutoweka, Mvuvi amewasomba, mtungoni kuwaweka,
Hakuna wa kumuomba, msamaha
kuutaka,
Leo wako mtungoni huzuni imewakumba.”
Pia katika shairi la “Bahari”
mwandishi anawapiga vita viongozi na watawala wanaowanyanyasa wananchi wenzao.
“Hudai ni haki yao, mola
amewajaalia,
Kuwadhulumu wenzao,
wao
Nao kwa unyonge wao, wadogo wateketea,
Bahari
ina hatari, wala usiichezee.”
Vilevile katika shairi la “Punda”
mwandishi anaelezea jinsi ambavyo watu wa hali ya chini wanavyoendelea kuonewa
na kuteswa kama Punda. Anaishauri jamii kukemea suala hili na kusaidiana
kuwainua wanyonge na sio kuendelea kuwanyonya.
“Toka ulipozaliwa, maishayo ni
kizogo,
Hujapata kuenziwa, waishi trigivyogo, Nawe
hujajielewa, u kiumbe hu kigo
Kama ungefadhiliwa usingebeba mizigo
Hakika ulionewa hustahili kipigo,
Haki
umeitambua, idadi japo kidogo”.
B;
FALSAFA
Falsafa ya waandishi wa mashairi ya
“Malenga wapya” ni kuwa jamii inaweza kubadilika kiuchumi na kupata maendeleo
kama itafanya kazi kwa bidii bila kuzembea, wanaamini kupingwa kwa utabaka na
unyonyaji ni suluhu ya amani na maendeleo. Wanaamini pia ukiishi vizuri duniani
utafanikiwa, wanasisitiza kutenda wema. Haki usawa na ushirikiano ni chachu ya
maendeleo.
C; MTAZAMO
Mtazamo wa waandishi ni wa
kiyakinifu kwani mambo wanayoyaeleza kama vile namna ya kutatua matatizo katika
jamii. Mambo wanayoyapendekeza yanawezekana kutimizika mfano uwepo wa haki,
kupinga utabaka, unyonyaji, kufanya kazi vizuri kuweka akiba na matumizi mazuri
ya pesa na mambo mengine mengi.
D; MSIMAMO
Msimamo wa kimapinduzi ni
msimamo wa waandishi wa diwani hii. Mambo wanayoyaeleza yanalenga kuleta
mapinduzi katika jamii mfano kupiga vita adui uvivu, kupinga dhuluma, kupinga
maovu yote. Hiyo ni ishara kuwa wanalenga kuibadilisha jamii. Wanatoa pia
changamoto na suluhu ya matatizo katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ya
kimaendeleo katika jamii kama vile kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia
maadili.
E ; UJUMBE
- Kufanya kazi kwa bidii ni chachu ya mendeleo
- Uaminifu katika ndoa, mapenzi ya kweli ni jambo la msingi
- Matumizi mazuri ya pesa husaidia kuwa na akiba nzuri na kupunguza umaskini
- Kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi, si budi kukithamini
- Kauli nzuri huepusha migogoro na chuki
- Kumkomboa mwanamke ni kuikomboa jamii, hivyo si budi kupinga tamaduni zinazomkandamiza
- Tunaaswa kupinga utabaka. Kutetea haki na kupuuza unyonyaji ili kuleta usawa katika maisha
- Viongozi walaghai na wasaliti hawafai kwa maendeleo hivyo tunaaswa kuwa makini kuchagua viongozi bora na kuwawajibisha
- wasiofaa.
Maswali ya mazoezi
1. Maadili mema na maonyo
yamejadiliwa na washairi wa diwani. Onesha mjadala huo kwa kutumia diwani
mbili.
2. Ni kwa vipi muundo na mtindo wa ushairi hutofautiana na muundo wa riwaya na tamthilya? Tetea jibu lako kwa kuonesha jinsi muundo na mtindo wa ushairi ulivyo.
3. Ujenzi wa taswira katika kazi za kifasihi hutufanya tuhisi au kuona kabisa uhalisia wa mambo ulivyo. Jadili kwa kutumia diwani mbili ulizosoma.
4. Waandishi wa kazi za fasihi ni walimu? Jadili.
5. Mtazamo, msimamo na falsafa ya mwandishi hututhibitishia ukweli wa mawazo yake katika kazi yake. Fafanua.
2. Ni kwa vipi muundo na mtindo wa ushairi hutofautiana na muundo wa riwaya na tamthilya? Tetea jibu lako kwa kuonesha jinsi muundo na mtindo wa ushairi ulivyo.
3. Ujenzi wa taswira katika kazi za kifasihi hutufanya tuhisi au kuona kabisa uhalisia wa mambo ulivyo. Jadili kwa kutumia diwani mbili ulizosoma.
4. Waandishi wa kazi za fasihi ni walimu? Jadili.
5. Mtazamo, msimamo na falsafa ya mwandishi hututhibitishia ukweli wa mawazo yake katika kazi yake. Fafanua.
Subscribe to:
Posts (Atom)